Taarifa ya Habari 19 Aprili 2024

Bango la taarifa ya habari la SBS Kiswahili

Waziri Mkuu ame sisitiza umuhimu wa mshikamano wakijamii nchini Australia, kufuatia uchunguzi kwa shambulizi lakigaidi la kudungwa kisu ndani ya kanisa wiki hii.


Mvulana mwenye miaka 16 amefunguliwa mashtaka ya ugaidi kufuatia uchunguzi wa polisi wa shirikisho kwa kisa cha shambulizi la kisu ndani ya kanisa moja mjini Sydney. Polisi wali itwa katika kanisa la Christ the Good Shepherd Church katika kitongoji cha Wakeley jioni ya Jumatatu Aprili 15, ambako inadaiwa Askofu Mar Mari Emmanuel alidungwa kisu mara sita wakati alikuwa akiongoza ibada iliyo kuwa ikipeperushwa mubashara mtandaoni. Kijana huyo kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi hospitalini, baada yakufanyiwa upasuaji kwa kidole chake kilicho katwa wakati wa shambulizi hilo. Kesi yake inatarajiwa kusikizwa ndani ya chumba anako lazwa hii leo, kesi hiyo ikiongozwa na mahakama ya watoto ya Parramatta.

Shujaa wa shambulizi la kisu katika soko la Westfields Bondi Junction, anatambuliwa na waziri mkuu ambaye amethibitisha kuwa mlinzi huyo mwenye asili ya Pakistan atapewa visa yakudumu nchini. Muhammad Taha alipelekwa hospitalin baada yakukabiliana na mshambuliaji huyo Joel Cauchi, alipokuwa akifanya shambulizi la kisu jumamosi ya Aprili 13 ambako watu sita wali uawa. Mfanyakazi wa mjengo kutoka Ufaransa, Damien Guerot naye alipewa visa yakudumu kwa matendo yake. Bw Taha aliomba kama naye anaweza pewa tuzo kama hiyo pia kwa juhudi zake.

Rais wa Kenya William Ruto Alhamisi jioni alitangaza kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Francis Ogolla, kilichotokana na ajali ya helikopta iliyotokea majira ya alasiri Kaskazini Magharibi mwa nchi. Akihutubia wanahabari katika ikulu ya Nairobi, Ruto alisema kuwa ndege hiyo ya kijeshi ilianguka eneo la Sindar kaunti ya Elgeyo Marakwet mwendo wa saa nane na dakika 20 alasiri. Ruto alisema watu wengine 9 pia walifariki katika ajali hiyo na kuongeza kwamba maafisa wengine wawili waliokuwa kwenye ndege hiyo walinusurika na wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Marekani imewazuia maafisa wanne wa zamani wa serikali ya Malawi kuingia nchini, kwa sababu ya kuhusika kwao katika ufisadi mkubwa, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Jumatano. Wanne hao walitajwa na Wizara ya Mambo ya Nje kama "waliotumia vibaya nyadhifa zao za umma kwa kupokea hongo na vitu vingine vya thamani" kutoka kwa mfanyabiashara wa kibinafsi ili kubadilishana na kandarasi ya serikali.

Nchini Uganda, wafanyabiashara jijini Kampala na miji mingine wanaendelea na mgomo baada ya kukataa wito wa serikali wa kufungua maduka yao. Wafanyakazi hao wanalalamikia mfumo mpya wa utozwaji kodi, wanaosema utawasababishia hasara. Waziri wa Fedha Matia Kasaija alitoa wito kwa wafanyabiashara hao kufungua maduka yao huku Serikali ikizingatia matatizo yao ndani katika muda wa wiki mbili zijazo.

Share